Safari ya Benjamin Netanyahu nchini Marekani; na madai yake dhidi ya Iran
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel ambaye amefanya safari nchini Marekani, siku ya Jumatatu alitoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Iran na kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, eti inaunga mkono ugaidi. Netanyahu ambaye amekuwa akiropokwa mara kwa mara na kutoa matamshi yasiyo na msingi wala ushahidi wowote dhidi ya Iran amesema kuwa, wanamgambo wa Kiislamu wa Kishia wanaoongozwa na Iran pamoja na kundi la Daesh wanataka kuikomboa Mashariki ya Kati (magharibi mwa Asia). Netanyahu aidha amesema kama ninavyomnukuu: "Mimi na Rais Obama tuna tofauti za kimitazamo kuhusiana na makubaliano ya nyuklia, lakini makubaliano haya yameshatiwa saini na sisi kwa sasa tunapaswa kuelekeza nguvu zetu katika suala la kutokiukwa makubaliano haya.” Mwisho wa kunuu. Nukta ya kichekesho katika matamshi hayo ya Waziri Mkuu wa Israel mbali na kuonyesha wasiwasi kuhusiana na makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 moja ni hii kwamba, Netanyahu ambaye yeye mwenyewe ni mshari na kiongozi wa ugaidi anaituhumu Iran kwamba, imeanzisha mitandao ya kigaidi. Hapana shaka kuwa, makubaliano ya nyuklia lilikuwa tukio lenye taathira na la kuzingatiwa. Tukio hili muhimu liliwafurahisha mno wapenda amani na wafuasi wa mazungumzo ya kimantiki kwa ajili ya kutatua hitilafu na mizozo. Hata hivyo katika upande wa pili wa sarafu jambo hili liliwafanya wasiotaka amani kuchanganyikiwa. Katika hili Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel ni mmoja wao, mtu ambaye tangu awali alihaha huku na kule kuonesha kwamba, makubaliano ya nyuklia na Iran ni hatari kubwa. Hata kama pirikapirika hizo za Netanyahu zilipaswa kutathminiwa katika fremu ya siasa za Israel za kuwahadaa walimwengu, lakini huu ni upande mmoja tu wa kadhia. Upande wa pili wa suala hili ni kwamba, mayowe na makele ya Netanyahu kuhusiana na Iran ni kuendelea siasa za kutapatapa na za kudakia mambo za utawala ghasibu wa Israel. Muamala huo wa Netanyahu unaweza kuwa stratejia yake muhimu kutokana na sababu kadhaa. Sababu ya kwanza ya Netanyahu kuzusha madai na kuendeleza propaganda dhidi ya Iran ni hii kwamba, mwanasiasa huyo mwenye misimamo ya kuchupa mipaka anahofia kubadilishwa mkondo wa mashinikizo ya kimataifa kutoka Iran na kuelekezwa Israel ikiwa ndilo dola pekee linalomiliki silaha za atomiki katika Mashariki ya Kati na ambalo halijajiunga na mkataba wa kuzuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia (NPT). Kwa hakika hofu ya kushadidi mashinikizo ya kutekelezwa mpango wa kulisafisha eneo la Mashariki ya Kati na silaha za atomiki ambao unapingwa na Marekani na Israel ni jambo linalomfanya Netanyahu atapetape na kuendeleza propaganda na madai yake katika uwanja huo. Sababu ya pili ya Netanyahu ya kung’ang’ania kuendeleza hilo ni mashinikizo yasiyokwisha ya Israel dhidi ya Marekani. Netanyahu amesema mara chungu nzima kwamba, ana wasiwasi kuhusiana na makubaliano ya nyuklia na Iran. Hata hivyo sababu ya wasiwasi huo inarejea katika masuala ambayo Israel inapaswa kutoa majibu na sio Iran. Hivyo basi, viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamekuwa wakitaka wapatiwe mambo mengi na Marekani kwa kisingizio kwamba, utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia na Iran yataigharimu Tel Aviv na kwamba, utawala huo utakuwa katika mazingira magumu. Matakwa hayo yanajumuisha kuongezwa misaada ya moja kwa moja ya kifedha kutoka dola bilioni 3 hadi 5 kwa mwaka sambamba na kupatiwa silaha zaidi jambo ambalo limebainishwa katika safari ya mara hii ya Netanyahu nchini Marekani. Tab’an, Marekani haina budi isipokuwa kutekeleza matakwa hayo ya Israel kutokana na umuhimu wa malengo yake ya kiistratejia katika eneo la magharibi mwa Asia ambayo yanafungamana na kubakia Israel. Sababu ya tatu katika kutathmini mwenendo huu ni wasiwasi wa Netanyahu wa kusambaratika hegomonia na mamlaka ya Magharibi hususan Marekani. Kile ambacho kimemtia kiwewe na wasiwasi mkubwa Netanyahu ni kusimama kidete Iran mkabala na vitisho, vikwazo na mashinikizo ya Marekani na kulifanya kundi la 5+1 likubali kuitambua haki ya Iran ya kunufaika na nishati ya nyuklia.
No comments:
Post a Comment