
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusiana na kuzidi kuzorota siku baada ya siku hali ya mambo katika nchi ya Burundi. Jeffrey Feltman’ Naibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kubainisha kuwa, Burundi inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa na kwamba, kuendea kwa kasi vitendo vya utumiaji mabavu katika nchi hiyo kutakuwa na matokeo mabaya kwa amani na uthabiti wa nchi hiyo. Zeid Ra’ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa na Adam Ding Mshauri Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari wote kwa pamoja wamelitahadharisha Baraza la Usalama la umoja huo kuhusiana na Burundi. Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, Burundi inakaribia kukumbwa na maafa. Tahadhari ya Umoja wa Mataifa na wasiwasi wa maafisa wa umoja huo katika masuala ya Burundi unaoneshwa katika hali ambayo, ripoti kutoka katika nchi hiyo zinaonesha kuongezeka mashinikizo na mivutano katika nchi hiyo. Kufuatia kukithiri mapigano na mauaji katika nchi hiyo, wiki iliyopita Rais Pierre Nkurunziza alitoa amri ya kukusanywa silaha zote zinazomilikiwa kinyume cha sheria na akawataka wapinzani kukabidhi silaha zao na badala yake wajumuishwe katika msamaha. Hata hivyo Rais Nkurunziza alitishia kwamba, endapo wahusika hawatakabidhi silaha zao watakabiliwa na mkono wa sheria na kuhesabiwa kuwa ni magaidi. Baada ya kumalizika makataa na muda wa mwisho uliotolewa na Rais Nkurunziza wa kukabidhi silaha, jeshi la polisi likitii amri ya Rais limeanzisha operesheni ya kuwapokonya silaha wapinzani ambapo operesheni hiyo hadi sasa imepelekea watu 9 kuuawa. Wachambuzi wa mambo wanaitathmini amri hiyo ya Rais Nkurunziza kuwa ni kupambana na wapinzani na kuwaua. Inasemekana kuwa, Rais Pierre Nkurunziza amelipa jeshi la polisi amri ya kufanya upekuzi nyumba hadi nyumba na kuwaua wapinzani na watu wenye kumiliki silaha. Licha ya kupita miezi kadhaa tangu kuzuka vurugu na machafuko nchini Burundi na kupelekea karibu watu 200 kuuawa na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi, lakini wimbi la machafuko na mauaji lingali linashuhudiwa ambapo akthari ya weledi wa mambo wana wasiwasi wa kutokea vita vya ndani nchini humo. Serikali ya Ufaransa ilitangaza nia yake ya kuwasilisha rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yenye lengo la kuzuia kushadidi machafuko nchini Burundi. Katika rasimu hiyo kumependekezwa kuwekewa vikwazo watu ambao wanahusika na machafuko ya nchi hiyo. Licha ya kutolewa tahadhari kuhusiana na uwezekano wa kutokea vita vya ndani na hata mauaji ya kimbari nchini Burundi, lakini Rais Pierre Nkurunziza ametupilia mbali uwezekano huo na kusisitiza kuwa, hakutatokea vita vya ndani na mauaji ya kizazi katika nchi hiyo na kwamba, serikali haitaruhusu hilo kutokea. Hata hivyo mauaji ya sasa dhidi ya wapinzani kwa kisingizio hiki na kile na kuzusha hali ya wasiwasi katika anga ya siasa ya Burundi ni jambo ambalo limehuisha kumbukumbu ya vita vya ndani vilivyowahi kutokea nchini humo na kupelekea maelfu ya watu kuuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. Vita hivyo ambavyo vilitokea kutokana na hitilafu na mizozo ya kikabila na ugomvi wa kuwania madaraka ya nchi hivi sasa inaonekana vikitokea kwa sura nyingine kwa kadiri kwamba, kama serikali na wapinzani hawatatua mgogoro wa sasa wa kisiasa kwa njia ya mazungumzo na katika anga tulivu kwa mara nyingine cheche za moto wa vita zitaibuka tena katika nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment